• Swahili
  • English
  • Mwanzo
  • Maswali/Majibu
  • Picha
  • Kuhusu sisi
  • Mawasiliano

HUDUMA ZA KLINIKI ZA KIFAFA KAMA ZIFUATAVYO

  • Uchunguzi wa Kitabibu
  • Kipimo cha EEG
  • Ushahuri nasaa
Hospitali ya Mt. Fransis - Ifakara
Siku za kazi:
Jumatatu, Jumatano, Alhamisi
Kuanzia 2:30 asubuhi hadi 9:30 Mchana
Mawasiliano:

0784 402 899 (Dr. Winifrid Gingo)
0693 842 402 (Dr. Mabusi)

INUKA Rehabilitation Hospital
Siku za kazi:
Jumatatu hadi Ijumaa
Kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi 9:30 jioni
Mawasiliano:

0759 951 085 (Reception)

0743 119 682
0784 592 237
(Dr. Godfrey Ligomba)

.
Iyunga Kituo Cha Afya
Siku za kazi:
Huduma zitaanza kutolewa kuanzia mwezi wa nane
Mawasiliano:

 

0789 643 786
0754 069 233
(Dr. Joshua Mwakyelu)

 

Je, Unamfahamu mtu yeyote mwenye Kifafa au anaepata Degedege?
Uonapo hali kama hizo fika katika Hospitali/Kliniki zetu kupata matibabu
Kama unamfamu mtu mwenye Kifafa au Degedege tufahamishe kupitia kurasa zetu za mitandao ya Kijamii, tutakusaidia kumuwezesha afike kwenye Hospitali/Kliniki zetu
Tufatilie kwa kubonyeza nembo ya mtandao itakayokupeleka kwenye kurasa zetu.

Maswali/ Majibu

Je, tunatoa huduma gani?

Tunatoa huduma kupitia Vituo mbalimbali vya afya vilivyobobea kwenye magonjwa ya kifafa.

Tumezindua Kliniki ya kifafa Ifakara mkoani Morogoro katika Hospitali ya rufaa ya Mt. Francisco pamoja na Hospitali ya INUKA ya utengamao, ilioko Wanging'ombe mkoani Njombe.

Kufikia mwezi Agosti tutatoa huduma hizo Jijini Mbeya katika kituo cha Afya cha Iyunga RC.

Kliniki zetu zina madaktari waliofuzu mafunzo ya kutibu kifafa, lakini pia tunatoa huduma ya kufanya kipimo cha EEG kupitia mashine maalum ambayo hutusaidia kutambua vyema aina ya kifafa ili kutibu kwa dawa sahihi. Hili ni muhimu sana kwa sababu kuna aina tofauti za kifafa na mara nyingi Wahudumu wa afya au wauguzi wa kituo cha Afya/Zahanati hutibu aina zote sawa kutokana na kukosa maarifa na uchunguzi sahihi.

Je, huduma zenu zinagharimu kiasi gani?

Kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mt. Fransisco, Ifakara kumuona daktari ni bure!
Lakini kipimo maalumu cha EEG kinachosaidia madaktari kutambua aina ya kifafa hutoza shilingi 25,000.
Ikiwa una bima ya Afya ya NHIF utapata huduma hii bila malipo.

Kwenye Hospitali ya Utengamao “Inuka”, iliyopo Wanging’ombe Mkoani Njombe, kumuona daktari ni shilingi 5,000 na kipimo cha EEG ni shilingi 30,000.
Kwa sasa bima ya NHIF haigharamii kipimo cha EEG, lakini tunalifanyia kazi.

Je Unaweza kuweka Ahadi na daktari?

Hapana, Hauhitaji kufanya ahadi na daktari

Naweza kupata njia za mawasiliano?

Hospitali ya Rufaa ya Mt. Francisco

0784 402 899 (Dr. Winifrid Gingo)
0693 842 402 (Dr. Mabusi) 

Hospitali ya utengamao “Inuka”
0759951085 (Mapokezi)
0743119682 (Dr. Godfrey Ligomba)

Kituo cha Afya Iyunga RC
0789643786 – 0754069233 (Dr. Joshua Mwakyelu)

Kifafa ni nini? Dalili zake ni zipi?

Kifafa ni hitilafu fulani inayotokea kwenye mfumo wa ubongo, ambapo shughuli za ubongo zinakuwa isivyo kawaida, na kusababisha degedege au hali au hisia fulani zisizo za kawaida, na wakati mwingine kupoteza ufahamu.

Dalili za kifafa, kama degedege, zinaweza kutofautiana sana na aina ya kifafa

  • Kutoa/ kukodoa/ kuchezesha kope za macho kwa sekunde chache;
  • Kukakamaa au kutetemeka mwili mzima;
  • Kupoteza fahamu kwa dakika/sekunde chache;
  • Viungo kukamaa;
  • Kushindwa kudhibiti viungo;
  • Kukamaa vidole vya mikono au miguu.
Chanzo kikuu kinachosababisha kifafa nini?

Mtu yeyote anaweza kupata kifafa, katika umri wowote: 

  • changamoto wakati mama anapojifungua kutopata elimu/huduma vizuri, mfano ukosefu wa hewa (mtoto kuchelewa kulia), hypoglycemia (kiwango cha sukari kuwa chini kwa mtoto);
  • kutokana na baadhi ya vimelea (Wadudu) kama vile Malaria na “Neurocysticercosis” (Minyoo itokanayo na nyama ya nguruwe isiyoiva vizuri);
  • vinasaba (kurithi);
  • ajali (majeraha kichwani);
  • matatizo yatokanayo na kiharusi;
  • uvimbe kwenye ubongo;
  • sababu isiyojulikana
Je, kifafa ni ugonjwa unaoambukiza?

Hapana. Mara nyingi mtu anapoanguka, hupoteza fahamu, na kupata degedege, tunapata hofu kumsaidia kwa sababu tunadhani inaweza kuwa kitu hatarishi na cha kuambukiza. Lakini hii si kweli hata kidogo.

Tafiti za kisayansi zinathibitisha kwamba mtu mwenye kifafa au anayepata degedege, hawezi kumuambukiza mtu mwingine. Tunapaswa kumsaidia ili arejee katika hali yake ya kawaida haraka iwezekanavyo.

Huwezi kuambukizwa kifafa kwa kugusa mate ya mtu aliyepata degedege.
Kifafa ni ugonjwa unaohusiana na itilafu fulani kwenye mfumo wa ubongo na degedege ni mojawapo ya dalili zake.

Je, kifafa ni laana?

Hapana. Kifafa huonekana kama laana kutoka kwenye mizimu ya mababu wakati mwingine kinahusishwa na mashetani.
Lakini pia inaaminika kuwa ni kwa sababu ya kurogwa na mara nyingi kuna dhana kwamba kinaambukiza.

Kifafa sio laana, bali ni itilafu kwenye ubongo ambayo hupelekea mtu kupata degedege kwa nyakati kadhaa.

 Je, kifafa kinatibika kwa tiba za asili?

Mtu anapopatwa na degedege kwa mara ya kwanza, mara nyingi wanafamilia hutafuta mganga wa kienyeji au kupiga ramri ili kujua inatokana na nguvu za giza au kutupiwa jini, roho za mizimu au sababu nyinginezo zisizo za kawaida. Mara zote familia hutumia gharama kubwa.

Nitamsaidiaje mtu wakati amepata kifafa?


Ukimuona mtu amepatwa na degedege, unaweza kuogopa, hasa ikiwa hujui nini cha kufanya. Kwa aina nyingi za degedege, hatua za msingi za huduma ya kwanza ndizo zinazohitajika.
Hatua za kuchukua ni rahisi na mtu yeyote anaweza kuzifanya:

  • kaa na mtu hadi degedege iishe na tazama degedege inadumu kwa muda gani;
  • ondoa vitu vyenye ncha kali karibu yake ili visi mjerui;
  • geuza kichwa cha mtu upande mmoja ili asikose pumzi, weka kitu laini chini ya kichwa chake;
  • usiweke kitu chochote mdomoni kwake kama vile maji, dawa, kibao au chakula mpaka mtu atakapopata fahamu;
  • Usimzuie anapokuwa akitetemeka;
  • kaa pamoja na mtu mpaka hali ya degedege itakapoisha;
  • mpeleke mtu hospitali ikiwa: 
    • degedege imedumu zaidi ya dakika tano;
    • degedege imejirudia mara kwa mara ndani ya siku moja;
    • alipata kifafa majini (bahari/mto);
    • ikiwa amepata majeraha au mjamzito;
    • ikiwa mtu harejei kwenye hali yake ya kawaida;
    • ikiwa ni mara ya kwanza kupatwa na hali hiyo.
Je, inawezekana kupona kifafa? Je, ninawezaje kudhibiti tatizo langu la degedege?

Kifafa kinatibika kwa dawa au wakati mwingine kwa upasuaji.

Dawa zinaweza kusaidia kudhibiti degdege na kupunguza idadi za kutokewa na degedege.

Baadhi ya watu hutibiwa kwa kipindi chote cha maisha yao ili kudhibiti degedege, lakini kuna baadhi degedege huisha kabisa na kifafa kupona. Baadhi ya watoto wenye kifafa, hupona kadri wanavyokua kiumri.

Mara nyingi watu wanakwenda kwenye vituo vya afya au zahanati zenye madaktari wasio na mafunzo ya kutibu kifafa na kupewa dawa zisizo sahihi, ambazo hazimsaidii mgonjwa inayopelekea familia na jamii kudhani kwamba kifafa hakitibiki kwa dawa za hospitalini. Ukweli ni kwamba kifafa kinatibika!

Kama unataka kujaribu huduma zetu, utakutana na madaktari wenye mafunzo na mashine maalum ya kutambua aina ya kifafa na utatibiwa kwa njia bora zaidi hatimaye kupunguza matukio ya degedege.

Picha

Kuhusu sisi

Comunità Solidali nel Mondo - ONLUS (Com.Sol)

ni Shirika lisilo la Kiserikali (NGO) la Kitaliano liliyoanzishwa mwaka 2007 na kusajiliwa rasmi nchini Tanzania kama NGO ya Kimataifa mwezi Mei 2017. Com.Sol imekuwa ikifanya kazi nchini Tanzania tangu mwaka 2010, katika mikoa ya Njombe, Mbeya, Dar es Salaam na Morogoro, kwa kushirikiana na mashirika ya Dayosisi ya Njombe, Dayosisi ya Mbeya Ofisi ya Maendeleo ya Caritas, Usharika wa Sista wa Ivrea, Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Francis na chuo kikuu cha SFUCHAS.

ComSol inakuza ustawi wa maendeleo ya jamii katika nyanja za afya, elimu, kilimo, na ajira kwa kuzingatia Watu Wenye Ulemavu (PWDs).

Mafanikio makubwa zaidi kwa miaka hii ni uzinduzi wa vituo vitatu vya utengamao vya kijamii (CBR) mkakati ni kuandikisha zaidi ya Watoto wenye ulemavu zaidi ya 7.000.

Kulingana na uzoefu wetu katika vituo vya utengamao, tumegundua watoto wengi wenye ulemavu pia wana kifafa.

Ukosefu wa vifaa na wahudumu wa afya wenye uwezo kutibu kifafa huongeza pengo kwa matibabu, na kwa kutotbu ugonnjwa huu kunazidisha ugumu wa maisha yao, shughuli za kujikmu na ufanisi kuhudhuria matibabu ya utengamao.

Ugonjwa huu pia umezungukwa na imani potofu na ukosefu wa elimu unaosababisha kuongezeka kwa unyanyapaa na ubaguzi.

Kwa hiyo, tumepanga mradi (Heri Walio na Huruma) unafadhiliwa na Italian Episcopal Conference (CEI) unalengo la kupunguza changamoto za kiafya na kijamii ambazo watu wenye kifafa wanakumbana nazo katika maisha yao ya kila siku.

Lengo letu la kwanza ni uzinduzi wa kliniki 3 za kifafa katika mikoa ya Mbeya, Morogoro na Njombe, kununua mashine ya EEG, kutoa mafunzo kwa madaktari watakaohusika na vituo hivyo, wahudumu wa afya kwa kila kituo, wahudumu na wenye kifafa wenyewe. Kwa msaada wa madaktari maalum kutoka Italia waliobobea katika magonjwa yanayohusiana na ubongo kwa Watoto (Child Neuropsychiatric).

Lengo la pili linahusu mafunzo ya wahudumu wa afya zaidi ya 200 katika mikoa 8 tofauti ya Tanzania kupitia mtindo wa mafunzo ya vitendo unaoongozwa na chuo kikuu cha SFUCHAS kuhusu usimamizi na taratibu juu  ya ugonjwa wa kifafa.

Shughuli hizo zinaongozwa na Profesa Senga Pemba, Profesa Albino Kalolo na Titus Mashanya.

Tunatumai inaweza kuwa kielelezo na kusababisha mpango mkakati wa kitaifa wa magonjwa ya afya ya akili, matumizi ya dawa za kulevya na hitilafu ya neva.

Lengo la tatu la mradi linahusu kampeni ya kitaifa ya kutoa uelewa na elimu kuhusu Kifafa kupinnga unyanyapaa kwa watu wenye kifafa miongoni mwa jamii kupitia njia tofauti (televisheni, redio na mitandao ya kijamii).

Kama sehemu ya mkakati wa CBR, lengo letu ni kuboresha hali ya maisha ya watu wenye ulemavu, na hasa wale wenye Kifafa na familia zao, ili kukuza ushiriki wao ndani ya jamii na kupunguza pengo la matibabu kwa kuboresha mfumo wa afya wa Tanzania.

Washirika

Wasiliana nasi

©  Kifafa Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa.